Matunda ya Ari Mpya na Nguvu mpya bila fikra mpya

13 11 2006

Nilitaka kusema, nikashikwa na kigugumizi lakini hata hivyo nilijikuta nasema ingawa nikashikwa mdomo na sheria ya kutoingilia mahakama, bali nadhani hakuna mahakama inayofanya kazi zake kisheria kufuata maoni na vishawishi vya watu wa mitaani.

Naamini mahakama zote zinafanya kazi kwa mujibu wa sheria na zinatoa haki kulingana na makosa husika bila kufuata ushawishi wa chombo chochote au maoni ya watu wa mitaani.

Hapa nina nia ya kulisema jambo hili ambalo magazeti ya Tanzania yamelivalia njuga kwa kipindi hiki ambacho serikali imepania kupigania haki za wanyonge kwa nguvu mpya kasi mpya na ari mpya.

Maskini Bro.Dito mtoto wa Ramadhani Mwinshehe wa Mzuzuri Born Town kitendo kilichomfika kinataka kuingia katika mkumbo wa kisiasa sijui kwa kuwa naye ni kijana kada aliyelelewa na siasa na kufika hapo alipo inasikitisha bali inaumiza familia ya Bin Mbonde ambaye amepoteza uhai wake bila hatia.

Hakustahili kuuawa bali sheria ya usalama barabarani ingefuatwa lakini si kama vile ilivyotokea kwa kiongozi mkuu kama Bro.Dito kuchomoa bastola na kumlenga shabaha dereva wa daladala kichwani.

Sijui ilikuwaje na wala sitaki kufikiria jinsi ilivyokuwa patashika kwaabiria waliokuwa wakiendeshwa na marehemu Mbonde wakati huo, mie nadhani walihisi basi limevamiwa na majambazi ambao hatimaye huenda wangeamrishwa kulala chini na kuvuliwa nguo zao.

Mie nadhani kilichofanyika hakikudiriki hasira kiasi hicho, au basi mkuu huyo angepiga risasi magurudumu ya gari lisiende mbele na hatimaye dereva angeshuka chini, bali kilichofanyika kwa kitendo cha kulipita gari kisha kulizuia lisiende na Mzee Dito kushuka kunako gari na kutoa cha moto.

Inatisha na nachelea kuendelea kusema kwa kile nilichokisema awali tumefungwa mdomo na sheria tuiache mahakama itende haki!!!!!!!!!

Ilianza kwa mkuu wa wilaya kumpiga mwenyekiti vibao, ikaja kwa RPC kuwatandika viboko wananchi imekuja kwa RC kuchomoa bastola na kumuua dereva wa daladala, itakuwaja kwa Waziri sijui atafanya nini….. na nanihii atafanya nini na nani hii atafanya nini mwishowe watu wataamua kujitoa muhanga ni hatari haki isipotendeka huu ni mtazamo wangu sidhani kama sheria inaweza kufuata mtazamo wa mtu na kuufanyia kazi.

Advertisements
Filamu iliyozua Utata

9 08 2006

Nadhani tukio la hivi karibuni la Mwana wa ‘Kukaya’Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ‘JK’ kulizungumzia suala la filamu ya Darwins Nightmare ya Bw. Hubert Sauper limechukua na kuhamisha fikra za wadanganyika.

Mimi nadhani watunzi wa riwaya na tamthiliya tutakuwa katika wakati mgumu kwa kuzuiwa kutoa kazi za kisanii na kifasihi kwa kuhofia dhana ya kuvuka mipaka ya fikra kwa matukio halisi yaliyopo.

Inakuwa ngumu kuchangia suala hili kabla ya kuiona filamu hiyo lakini kikubwa ni kwamba utunzi wa tamthiliya ni ubunifu wa kisanii uliochagizwa na fikra binafsi za mtunzi kwa mnasaba wa matukio halisi yanayojiri katika jamii.

Hebu wanablogi waliobahatika kuiona filamu hiyo watudadavulie yaliyomo ndani ya filamu hiyo ili tuanze kuchanganua kilichopo tujue pumba zipi na mchele upi, naamini,akina Sultani Tamba na wengine waliomo ndani ya Blogi wataungana nami kulichangia hili.

Wakatabahu

Fasihi(Matumizi ya lugha kwa wasanii wa kizazi kipya)

29 07 2006

KISWAHILI ni miongoni mwa lugha zilizojichukulia sifa lukuki kwa makuzi yake katika nnnchi za Afrika mashariki, Afrika na ulimwengu kwa ujumla ambako kukua kwake kumechangia kwa upande mmoja ama mwingine kukuza maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.

Kutokana na kukua kwa lugha hii si aghalabu kuwasikia jamii ya watu wenye asili ya Kiafrika kuitangaza na kuitumia katika matumizi yao kama vile kwa njia ya usanii na vinginevyo.

Nimepata kumsikia msanii mmoja mwenye asili ya Kiafrika Michael Jackson akitumia vionjo vya lugha ya kiswahili katika moja ya nyimbo zake jambo linalotia moyo kwamba lugha hiii ikitangazwa kwa njia ya sanaa inaweza kuenea na kusambaa ulimwenguni kote.

Michael Jackson,mwanamuziki wa Kimarekani mwenye asili ya Kiafrika katika wimbo waake wa ‘Liberian Girl’ ametia vionjo vya ‘Nakupenda pia!!nakutaka pia!! Mpenzi wee!!!’

Ajabu kwa wanamuziki na wasanii wa muziki wa kizazi kipya wa hapa nchini ambao mara nyingi wanatumia nyimbo zao kwa mtindo wa fasihi simulizi, kwa kuigiza na kutunga tenzi na mashairi yasiyo na vina wala mizani sawia aambapo badala ya kutunga nyimbo zenye mantiki hutumia uwanja huo kwa kuimba nyimba ambazo hazina ujumbe wala kuifundisha jamii.

Utasikia mwanamuziki anaimba,”Twenzetu tukapige ulabu tukishakuwa Bwax tenzetu Klaabu tukacheki wachumba na mademu bomba”.

Maneno ylaiyomo katika ubeti huu wa moja ya nyimbo nyingi za wasanii wa muziki wa kizazi kipya hazifundishi lolote zaidi ya kuchochea ulevi na hamasa ya vitendo vya ngono ambapo hapo awali malenga na waimbaji wa zama hizo walitumia fursa yao katika nyimbo kuelimisha jamii.

Mie nadhani kuna haja ya hawa wasanii wa kizazi kipya kubadilika ili kwenda kwa mnasaba wa matakwa ya wadau wa lugha ya kiswahili ikiwa ni pamoja na kuchunga nidhamu ya lugha na muonekano wake kwa jamii.

Wakatabahu

Fasihi(Kisa Cha Mtema Kuni)

28 07 2006

Swala linanitatiza, kisa cha mtema kuni,
Ni lipi lilomkwaza, kwa kumtaja vinywani,
Akatufanya kuwaza, mtema kuni ni nani,
Kisa cha mtema kuni, alifanyani?

Kisa cha mtema kuni, ni kauli ya zamani,
Wahenga walibaini,kisa chake kwa undani,
Sisi akhiri zamani,hatukimanyi yakini,
Kisa cha mtema kuni, alifanyani?

Katika kutema kuni, kilichomsibu nini?
Alikutana na nini,alipofika porini?
Au watu wamebuni, kufurahisha uneni?
Kisa cha mtema kuni, alifanyani?

Nilidhani akilini, alipotea mwituni,
Baada kutema kuni, katumbukia shimoni,
Hakutokea nyumbani, mwisho wa mtema kuni,
Kisa cha mtema kuni, alifanyani?

Nilibuni fikirani,alikutana na jini,
Kapelekwa baharini,akazamishwa majini,
Baada ya siku tisini,akarudishwa nchini,
Kisa cha mtema kuni alifanyani?

Mambo mengi nilidhani, juu ya mtema kuni,
Kakata mzeituni, ukanena ewe nani?
Ukamkwida shingoni,mbio akazisaini,
Kisa cha mtema kuni,alifanyani?

Swala hili si utani, limenikwaza amini,
Nalianika ugani, msawiri bloguni,
mtafakari makini, wa Mrima na wa Pwani,
Kisa cha mtema kuni, alifanyani.

Nahitimisha uneni, wasomaji bloguni,
Naomba nipokeeni, jawabu lenye mizani,
Makene wa kasirini,na wengine duniani,
Kisa cha mtema kuni asili yake ni nini?

Shairi hili niliwahi kuliandika katika magazeti ya Mwananchi Juni 23 2001 na Nipashe Juni 19 2001 lakini hadi sasa sijapatiwa jibu nimeamua kulikariri katika blogu asaa huenda nitapatiwa jibu la kuniridhisha.

Wakatabahu.

FASIHI(TUJADILI MILA NA DESTURI HIZI)

19 05 2006

KUNA jambo moja la kimila sijui ni la kidesturi za Kiafrika ama sijui ni ustaarabu wa watu wa ukanda fulani wa sehemu katika nchi yetu linanitia kichefuchefu, hata hapa ninapoanza kupandisha mada hii najihisi kama nimelemewa na mzigo mzito wa maji ‘aka’ mate uliojaa kinywaji kwa minajili ya kutaka kutema ‘aka’ kutapika kwa kujihisi vibaya.

Si kwamba labda binti fulani rafiki yangu kanibebea mimba ndio maana najisikia hivi, kwani kuna itikadi kwamba kama mwanamke uliyekaribu nawe hata kama si Girl Friend wako ‘aka’ mpenzi wako, ana ujauzito anaweza kukuambukiza wewe tabia na mienendo ya hatua zote za ujauzito ikiwa ni pamoja na kupenda kula vitu vyenye ugwadu, udongo n.k.

Kinachonitia kichefuchefu si hilo, bali tabia hii ya baadhi ya watu wa aina fulani katika mila za kiafrika…eti siku ya kumuoza binti yao ili kuthibitisha kama binti huyo alikuwa bado ni BIKRA humualika kungwi ambaye atakuja kushuhudia tendo la ndoa linavyotendeka na yeye kutoa taarifa kwa wahusika kama binti yule alikuwa mzima ama la.

Kwamba siku hiyo mara baada ya kufungwa kwa ndoa mume na mke huandaliwa chumba maalumu mchana kweupe, kukiwa na mashuhuda anuai na kisha hutandikwa kitambaa cheupe katikati ya kitanda kwa minajili ya kuangalia rangi nyekundu (aka) damu ambayo itathibitisha kwamba binti huyo hakupata kuingiliwa kimwili katika maisha yake hadi siku hiyo ya ndoa.

Eti husemwa kuwa mume anapomuingilia mkewe iwapo bado ni BIKRA haruhusiwi kumalizia ndani kwa ndani na kwamba eti yule kungwi ndiye anachukua mamlaka ya kuwa mke kwa muda ule ili kummalizia ashiki zake yule mume(sina ushahidi nalo hilo), lakini kwa yale niliyoyashuhudia kwa mboni zangu mbili zinanifanya nione mila hizi zinatia kichefuchefu na wala hazifai kufuatwa.

Kwamba mara baada ya kujulikana kwamba yule Binti alikuwa ‘MWALI’ basi shangwe vifijo na vigelegele hurindima na kupigwa mbiu kwamba, ndoa imejibu ambapo mama ‘Mzaa Chema’ hupakwa unga mweupe (sijui kwa mila zingine hufanya vipi) na kisha eti mama huyo hupewa tuzo fulani ikiwa ni sehemu ya shukrani za kumtunza bint yake hadi kufikia kuolewa bila kuingiliwa na mwanaume yoyote.

Ukiangalia kwa makini hali ya binti kujitunza na kufikia hatua ya kuolewa kabla ya kuguswa na mwanamume inaleta hamu ya kuisifia hali hiyo na kutoa pongezi hususani katika kipindi hiki kilichozongwa na maradhi ya ugonjwa wa UKIMWI, lakini zile hatua zinazochukuliwa kubani kwaamba binti huyu ni BIKRA zina walakini.

Nina mengi ya kuelezea juu ya hili heebu niwaachie wambuji wa kuchangia mada uga wao(Haya na tuchangie hili na ikiwezekana ipatikane njia mbadala badala ya hiyo iliyopo sasa)

Chemi Che Mponda, Martha Mtangoo, Zainabu Yusuf, Fatma Karama[MM1] , hii ni changamoto kwenu tuelezeni kama njia hii ina manufaa yoyote kwa akina dada ama ni udhalilishaji.

Wakatabahu.

FASIHI SIMULIZI(SIMULIZI YA KISAYANSI)-SCIENCE FICTION

15 04 2006

Bw. Makene hii ni sehemu ya kazi ambayo imenifanya niwe mvivu kupannndisha kazi za kishairi katika Blogu

RASI YA DHULUMIKA-1.

Na, Rashid Mkwinda.

CHOMBO kilikuwa kikikata mawimbi katikati ya bahari kuu usiku wa manane huku mawimbi ya bahari yakikilazimisha chombo hicho kufuata muelekeo sanjari na mawimbi hayo yaliyosababishwa na bamvua ambapo samaki wakubwa aina ya Papa na Nyangumi nao walijificha katika Matumbawe ya bahari wakiipa nafasi bahari kukamilisha mchafuko wake.

Giza lile totoro liliongeza hofu kwa mabaharia waliokuwemo ndani ya chombo ambacho kwa wakati huo kilionesha dhahiri kulemewa na misukosuko ya bahari huku Nahodha akijitahidi kwa kila hali kukinusuru chombo na mabaharia waliokuwemo kutokana na dharuba ile kuu ya Tsunami.

Kila aliyekuwemo katika chombo kile alihaha kunusuru maisha yake ilhali wasafiri ambao wengi wao walikuwa hawajui kuogelea wakiwa wamekumbatiana kila mmoja akiomba dua na uokovu na nusura ya Muumba wake ili aokolewe na gharika ile.

Hatima ya gharika ile iliwanusuru Baharia mmoja ambaye alishika kipande cha ubao na mwanamke mmoja ambaye aling’ang’ania guduria kubwa ambalo lilitumika kwa ajili ya kuhifadhia maji ya kunywa ambalo alielea nalo baharini kwa siku sita mtawalia.

Kila mmoja kati ya wahanga hawa wa Gharika la Tsunami ambalo ulikuwa ni mchafuko uliotokana na mtetemeko wa ardhi wa chini ya bahari alipata adha na shida ya aina yake ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha na mali zilizokuwemo ndani ya Chombo.

Baharia ambaye kwa wakati huo alikuwa hoi akitarazia msaada wa kuokolewa kutoka katika Zilizala ile aliangaza pande zote kiasi cha upeo wa macho yake katika bahari kuu iliyojaa ukiwa huku Ndegemaji na wengine walao samaki wakitarazaki chochote baharini ambacho aidha kimesazwa na kizaazaa cha Tsunami au vinginevyo.

Alijaribu kutafakari maisha yake baada ya hapo na jinsi ambavyo angeweza kujiokoa katika balaa lile ambapo baadaye alijikuta akikosa nguvu na kukata tamaa ya kuendelea kuishi duniani kutokana na njaa na kiu alivyodumu nayo siku sita.

Nguvu zilimuishia, tumbole liliingia ndani kutokana na kukosa chakula, alishindwa hata kupata nguvu ya kumudu kusukuma pumzi zake,viini vyeusi vya macho yake vilianza kupanda juu, nuru ya macho yake ilianza kupotea na hivyo alianza kuona giza mbele yake….. taratibu viungo vyake vilikosa nguvu …alijiona yuko katika dakika za mwisho za uhai wake.

Baharia aliishiwa nguvu na kujikuta akikata tamaa ya kuendelea kuishi aliinama chini na kutafakari namna kifo chake kitakavyomkabili na jinsi atakavyokuwa chakula cha Papa na Nyangumi baharini alijikuta akidondokwa na machozi ambayo hata hivyo, hayakuwa na muombolezaji.

Alitafakari kwa makini mustakabali wake na kujiona ni mmoja wa watu waliokosa thamani chini ya anga hili,jambo moja pekee alilolikumbuka katika hali ile ya kufa kufa aliona ni kumuomba Mwenyezi Mungu amfishe ilhali akiwa ni miongoni mwa waja wema waliopata kuishi katika dunia hii.

Hivyo alitumia fursa hiyo kuungama makosa yake yote aliyoyafanya katika mazingira ya kidunia ili aweze kuishi vyema baada ya kifo chake.

Chini alijiinamia,
Dhambize kufikiria,
Mwishowe kuufikia,
Alilia Baharia.

Tama alijishikia,
Kwa kifo kukabilia,
Shida ilomkutia,
Ganzi alijisikia.

Kwa yake tafakuri,
Hakutarazi Saburi,
Mwokozi hakujiri,
Kwa dunia kuhajiri.

Moja alilokiri,
Kufa kifo cha bahari,
Lisionekane kaburi,
Samaki waule mwili.
.

Akiwa katikati ya mawazo na tafakuri nzito aliinua macho yake juu na kumuona kiumbe mmoja mrefu ambaye urefu wake ulitaka kukaribia kufika nusu anga mawinguni huku akiwa amesimama juu ya maji bila kuzama alimfuata baharia sanjari na muelekeo wa upepo wa bahari ulivyovuma.

Alimtazama kiumbe yule wa ajabu kwa hofu huku akitetemeka na kuendelea kutafakari upweke alionao huku akiwakumbuka wenzi wake waliohiliki katika dharuba ile ya Tsunami, kiumbe yule aliendelea kumkaribia Baharia kwa kasi ya ajabu huku baharia akiendelea kuingiwa na hofu kuu juu ya aina ya kifo chake kitakavyojiri.

Kiumbe yule alitembea juu ya maji kwa mwendo wa kasi, hatua moja sawa na hatua thelathini za binadamu wa kawaida, hofu kuu ilitanda katika moyo wa Baharia akijua mwisho wa maisha yake umewadia huku njaa na kiu vikimuandama kwa siku sita alizokuwa akielea baharini.

‘’Bora nijifie majini kuliko kufia mikononi mwa kiumbe huyu wa ajabu’’ alijisemeza Baharia huku mikono yake ikikosa nguvu na kujikuta akiachia ubao uliokuwa ukimsaidia kuelea nao majini,akajikuta akitumbukia baharini na kuanza kutapatapa majini huku akinywa maji ya bahari yaliyokoza chumvi chumvi na hivyo kumuongezea kupiga chafya mfulufulizo.

Kila alipokuwa akiachama mdomo wake kwa ajili ya kupiga chafya ndivyo ambavyo alizidi kunywa maji na hivyo kuhitimisha ile azima yake ya kuelekea safari ya kifo, taratibu alihisi Izraili mtoa roho akikaribia kuitoa roho yake alifumba macho yake ili asisikie machungu ya kutokwa roho, kwani alipata kusikia kuwa mtoa roho pindi anapotoa roho maumivu huwa ni makali kadhalika hushikwa njaa na kiu.

Kwa wakati huo yule kiumbe wa ajabu alikuwa amekwisha karibia alipo Baharia na wakati huo anajiachia kutoka katika kile kipande cha ubao ambao alikuwa akielea nao kwa siku sita alitanguliza kiganja chake kipana chini ya bahari na kukitawanya.

Baharia alijikuta akitua katika kiganja cha kiumbe yule wa ajabu na kwa kasi ileile akajikuta akipaa hewani juu na kushuka kwa kasi moyo wake ukimpaa na tumbo lake tupu ambalo lilikuwa halijapata chakula kwa siku sita likiunguruma kutokana na mshituko wa kupaa mithili ya mtu aliyepanda ndege au meli iliyokuwa ikisukwa sukwa na mawimbi.

Alipaa hewani mithili ya mtu aliyeko ndotoni ilhali akiwa amelala huku akiwa amenyoosha miguu yake ghafla akajikuta yuko katika ardhi nzuri yenye majani ya rangi ya kijani kibichi iliyokuwa na dalili ya kusheheni kila aina ya matunda na vyakula, ndege wa rangi mbali mbali waliruka huku na huko na kutoa mandhari nzuri ya sehemu ile iliyoambatana na manukato ya maua mazuri yaliyomo katika ardhi ile.

Baharia alijaribu kutafakari kama yumo ndotoni au yuko katika hali yake ya kawaida, alijaribu kurudisha fikra zake nyuma juu ya gharika waliyoipata baharini na baadaye kuokolewa kwa kujishikiza katika kipande cha ubao ambacho alielea nacho kwa siku sita na baadaye alichoka na kuamua kukiachia kibao huku akiwa amemuona kiumbe yule mrefu.

Akiwa katika tafakuri ile alihisi huenda alikuwa amekufa na yule kiumbe aliyemuona ndiye malaika mtoa roho za watu yaani Izraili na kwamba huenda pale alipo ni peponi, lakini jambo moja lilimpa shida katika mawazo yake,kwamba kwa wema gani alioufanya duniani apate malipo ya kukaa katika pepo nzuri kama ile?

Kwani ile ardhi ilikuwa inameremeta nuru ya vito vya thamani na ilipendeza kwa rangi ya maua yake sanjari na ndege, Popo wenye rangi nzuri ambao walikuwa wakivinjari huku na huko wakifurahia ardhi ile ambayo ilionekana imejaa amani na utulivu wa asili kutoka enzi na enzi tangu ilipoumbwa dunia.

‘’ Hivi mimi niko ndotoni au ni hali halisi inayonitokea hapa nilipo? Au hapa ndio peponi? Alijisemeza moyoni.

‘’Lakini peponi ni sharti kwanza ufe na baadaye ufufuke na kuhesabiwa matendo yako ikiwa ni wa kwenda peponi au motoni, lakini mimi mbona sikumbuki kama nilikufa kwanza na baadaye kufufuka, au inawezekana pale nilipokutana na yule kiumbe wa ajabu?

‘’Mhh!! Yule ndiye mtoa roho za watu Izraili….. kweli nilikufa …nilizama majini….nilijiachia majini nikafia majini…nilijikuta nikipaa hewani na kufikia hapa nilipo’’ Alijiuliza kimoyomoyo Baharia.

Alijikuta akiwa katika utata mkubwa wa fikra… ‘’Inawezekana kweli nilikufa na baadaye kufufuka lakini mbona sikumbuki kama kuna mema niliyoyafanya yanayolingana na malipo ya kuishi kwenye bustani nzuri kama hii? aliendelea kujiuliza ndani ya moyo wake.

Hatimaye alihitimisha fikra zake kwa kuamua kubaki na moja kuwa huenda alikufa na hapo ndipo pale ambapo viongozi wa dini walikuwa wakipaeleza ndani ya vitabu vya dini.

‘’Huenda yule ni malaika miongoni mwa malaika wa peponi’’ aliendelea kujisemeza moyoni mwake yule Baharia.

Akiwa katika kutafakari hali ile mara alimuona yule kiumbe wa ajabu akiwa amesimama mbele yake huku akiwa ameshika matunda yenye rangi nzuri, kwa hali aliyokuja nayo yule kiumbe wa ajabu Baharia alibaini kuwa alikuwa ni mwokozi wake na kwamba alikuwa ni miongoni mwa wa viumbe wema.

Alimsogelea yule kiumbe na kisha akapokea yale matunda na kwa haraka na pupa ya njaa aliyodumu nayo kwa takribani wiki nzima aliyatia mdomoni, baada ya kubaini ladha ya matunda yale hisia zake zikachanganyika na nguvu ya ajabu na kujiona mithili ya mtu aliyezaliwa upya.

Alijihisi kama mtu aliyeongezewa nguvu kimiujiza,alirejea na nguvu kushinda ile ya awali na kujikuta akiwa na siha nzuri kiajabu.

Pamoja na neema aliyokuwa nayo lakini katika kisiwa kile alikuwa pekee yake, hakuwepo binadamu yoyote, kisiwa kilisheheni kila aina ya matunda ambayo yalikosa mlaji, ardhi ya kisiwa kile ilisheheni madini ambayo hayakuwa na mtumiaji.

Aliishi katika upweke ule kwa takribani miaka miwili, siku moja akiwa katika matembezi yake ya kawaida kisiwani mule alitokewa na msichana mmoja mrembo ambapo kutokana na hali ya upweke aliyokumbana nayo kwa miaka miwili alidhani yule aliyemuona alikuwa si Binadamu bali ni kiumbe wa Kijini.

Alijiona kama yuko ndotoni alijaribu kufikicha macho yake na kuangalia vizuri bila kuyaamini macho yake hadi pale yule msichana alipokaribia na kumsabahi kwa lugha fasaha ya kiswahili nyororo na mwanana.

Binti yule akafarijika na kuijibu kwa pupa na kutaka kumjua yule msichana aliyemuona kama ni binadamu au Jini yule msichana alimtoa hofu baharia na kumueleza namna alivyofika pale kisiwani.

Alieleza jinsi alivyokuwa abiria katika meli iliyopata dharuba na jinsi alivyookoka kwa kushikilia guduria kubwa la maji baharini, akiwa katikati ya bahari hali ya kuwa kiu na njaa imemshika barabara alijiona tayari mtu wa kufa kwani hakutarajia msaada wowote.

Alipojiona amechoka akaliachia lile guduria la maji liende zake naye akaanza kuzama kwa kasi huku pumzi zikiwa zinampaa.

Mara akajikuta ametua kwenye kitu mfano wa godoro kubwa, alipotua tu, akarushwa juu kwa kasi na kujiona anaelea katika anga la nchi kavu, taratibu akaanza kuteremka ardhini na kutua katika nchi yenye manukato ya marashi yenye mimea mizuri rangi ya Chanikiwiti inayovutia na kila dalili ya rutuba.

Aliwaona ndege na Popo wakivinjari katika maua yenye rangi maridhawa, mara akamwona kiumbe wa ajabu mbele yake akiwa ameshika matunda katika kiganja chake kikubwa, awali alimuogopa kiumbe yule lakini kutokana na njaa aliyokuwa nayo alimsogelea yule kiumbe ambaye alikuwa mrefu kupita mnazi.

Alipomsogelea akampa matunda na kuyatia mdomoni kwa pupa, aliyala yale matunda kwa pupa kutokana na njaa aliyokuwa nayo, mara alipokula alirejea katika siha yake njema kama awali, ndipo alipoanza kuzunguka huku na kule ndani ya kisiwa bila kumuona kiumbe yoyote wa mfano wake.

Binadamu pekee aliyekuwa ndani ya kisiwa kile alikuwa ni Baharia, ingawa hawakukutana na msichana yule na hivyo kila mmoja kujiwekea makazi yake katika kisiwa kile akitarazaki kwa matunda na kuishi mithili ya mnyama kutokana na kukosa mavazi.

Binadamu wale walionekana na afya njema ingawa viungo vyao vilikuwa wazi sehemu kubwa isipokuwa katikati ya mapaja na magoti na kwamba jambo pekee lililodhihirisha utu wao ni kuweka stara kwa kuvaa majani sehemu zao za utupu.

Mavazi waliyokuwa nayo awali yalichakaa kabisa mwili laini na mororo na sura nzuri ya msichana yule ulimvutia sana baharia bila kutarajia akajikuta anamsogelea na kumshika mabega yake huku akiisawiri vyema sura yake maridhawa.

Kama mtu aliyekumbuka jambo fulani ghafla akamwachia yule msichana na kuanza kutafakari ni wapi amewahi kumuona yule msichana mwishowe akakumbuka kuwa alikuwa ni mmoja wa abiria waliokuwemo ndani ya ile meli iliyohiliki.

Msichana naye kwa upande wake aliikumbuka vyema sura ya baharia yule ijapokuwa alibadilika kutokana na nywele ndefu nyingi alizokuwa nazo wajihi wake ulimkumbusha yule msichana kutokana na ucheshi aliokuwa nao ndani ya chombo kilichohiliki.

Alikuwa na kawaida ya kuwaburudisha abiria ndani ya chombo kwa kuwakariria mashairi mbalimbali, yule msichana akamsogelea baharia na kumkumbusha baadhi ya ya beti za mashairi alizopendelea kughani;

Twaomba mola karima,
utujalie uzima,
utufikishe salama,
katika yetu safari,
kwako ndiko twaegemea,
kwa kila lililo jema.

Ewe ndiwe mwenye dhima,
kwa kila kheli na shari,
Mola wetu muadhama,
muumba nchi na sama,
tuepushe zahama,
dua kwako twaombea.

Kwa zako nyingi karama,
twatarajia salama,
tufike nyumbani vyema,
jamaa kusalimia.

Mirindimo ya sauti ile nyororo ilimvutia sana yule baharia akajikuta akitabasamu na kuyumbayumba huku na kule mfano wa mtu anayeyumbishwa na mawimbi akiwa ndani ya chombo,Baharia alifurahi upeo wa furaha yake kwani alikumbushwa enzi za kazi yake ya ubaharia.

Akainuka na kumkumbatia yule msichana kwa furaha kubwa wakiwa katika kukumbatiana mara wakasikia upepo mkali mfano wa kimbunga ukipuliza kwa kasi hali ile iliwafanya wazidi kukumbatiana wakihofia kuzolewa na kile kimbunga na kutupiwa baharini.

Mara upepo ukatoweka na viumbe wawili warefu wakawa wamesimama kwa upande wa kila mmoja,mmoja alisimama upande wa Baharia ilhali mwingine upande wa yule msichana,Baharia alimkumbuka vyema yule kiumbe mrefu kwani ndiye aliyemuokoa naye yule msichana alimkumbuka yule kiumbe kutokana na kumpa matunda yaliyomrejesha katika hali yake ya awali.

Yule msichana akaelezwa jinsi alivyookolewa wakati akizama majini, wakati msichana yule yuko hatarini alitanguliza kiganja chake kikubwa chini ya bahari ambapo mara alipo tua tu katika kiganjani alimrusha angani kisha akamteremsha ardhini taratibu na baadaye akamtokea akiwa na matunda mkononi.

Alisema alifanya vile kwa kuchelea kujitokeza machoni kwa msichana yule akiwa kule baharini kwa kuhofia kumtia kiwewe hali ambayo ingeweza kumsababishia kifo kutokana na maumbile yao wale viumbe yalivyokuwa ya kutisha pia kutokana na uchovu wa njaa na kiu aliyokuwa nayo yule msichana, vile vile kutokana na mioyo ya wanawake ilivyokuwa dhaifu.

Na kwamba hiyo ni moja ya sababu zilizo mfanya ajitokeze katika hali kama ile huku akiwa ameshika matunda ili kuonesha namna ya upendo aliokuwa nao juu yao.

Baadaye wale viumbe wakajieleza kuwa wao ni viumbe wa Kijini ambao walitokea karne nyingi zilizopita katika Milki ya Mfalme Suleiman na kwamba kutokana na kukaa muda mrefu katika kisiwa kile na jinsi walivyokula chumvi nyingi wakawarithisha Baharia na yule msichana kila kilichomo ndani ya visiwa vile na kuwaombea dua na baraka kwa kila watakacho kichuma kutokana na mikono yao.

Baadaye wale viumbe Wakijini waliowaozesha Baharia na yule msichana wakaishi wakiwa kama mtu na mkewe wakajaaliwa kupata watoto wengi ambao walikuwa mapacha wa kike na kiume nao waliendelea kuzaliana hadi kufikia kujaza kisiwa na kuwa watu wengi ambao walitokana na Baba na mama mmoja na wale viumbe wa Kijini walitoweka na kisiwa kile kikawa na watu wengi kutokana na kizazi kile cha Baharia na mkewe.

………………………………………………………………………………………….

DANGANYIKA na Fitinika ni miji iliyopo katika kisiwa kimoja ambapo Baina ya miji hiyo kulikuwa na mfereji mdogo ulioigawa miji hiyo awali watu wa upande mmoja walivuka upande wa pili kwa kutumia kidaraja kidogo kilichokuwepo hapo.

Kadri siku zilivyoyoyoma ndivyo mfereji ule ulivyoongezeka ukubwa na kuwa kama mto, daraja ya kuvukia upande wa pili ikaongezwa urefu, mto ule ulipanuka mwaka hadi mwaka na kukigawa kabisa kisiwa kile kuwa ni visiwa viwili vilivyoko umbali mrefu.

Na kadri miji ilivyozidizidi kuwa mbali uhusiano baina ya pande hizi ulipungua na kwamba ilikuwa ni nadra kutembeleana kama hapo awali seuze kujuliana hali baina ya watu wa visiwa hivi ambao kwa asili walikuwa ni ndugu wa kuzaliwa.

Jinsi ufisadi ulivyozidi katika ardhi ndivyo ambavyo umbali baina ya Danganyika na Fitinika ulivyoongezeka,baadaye ilibidi wale watu waliokuwa na uwezo ndio ambao waliweza kufanikiwa kwenda kisiwa cha pili kwa kutumia vyombo vyao vya kasi.

Hatimaye hata hivyo vyombo viendavyo kasi vilitumia siku saba majini hali hii iliwatia hofu wasafiri ndani ya bahari na hatimaye mawasiliano ya kindugu baina ya visiwa hivi yakaanza kutoeka kadri siku zilivyokwenda.

Wimbi la ugeni kutoka nchi za kigeni ulianza kuviathiri visiwa hivi taratibu wageni kutoka katika nchi za ughaibuni walivivamia kwa kasi visiwa hivi,wakiwa wamevutiwa na utajiri na mali ya asili iliyopo ndani ya ardhi ya visiwa hivi.

Maadili ya wakazi wa visiwa hivi yalianza kumong’onyoka kutokana na kufuata mila za wageni wavamizi, kutokana na utajiri uliopo wavamizi walijikuta wakilowea na kuhodhi mali zote za visiwa, ili kuwateka wakazi wa visiwa hivi wageni waliwashauri kuunda umoja baina ya pande mbili za visiwa.

Viongozi wa ngazi za juu waliupokea ushauri huu kwa mikono miwili, na hivyo kujikuta wakianza kuwatumikia wavamizi kwa kila hali ambapo walitumia fursa hiyo ya kukubalika kwao miongoni mwa Viongozi wa Visiwa hivi kupanga mbinu za uhujumu na ufisadi dhidi ya rasilimali iliyopo.

Wageni walipanga mbinu kupitia umoja huo ili kuvinjari pande zote za visiwa bila vikwazo vyovyote, ambapo walitumia mbinu hizo kuwekeza vitega uchumi baadaye wakaanza kuweka vitega uchumi mbalimbali visiwani humo kutoka Ughaibuni kila kukicha.

Tabia za wenyeji zikaanza kubadilika kwa kufuata mila za kigeni ambapo nao wakautumia mwanya huo kupandikiza fikra zao na kuhamisha kila rasilimali na kupeleka kwao huku wenyeji wakijisahau kutokana na vijizawadi vidogo vidogo.

Walibeba mali nyingi vikiwemo vito vya thamani ambavyo kwavyo walitengeneza za vidani ambavyo baadaye walikuja kuviuza kwa wazalendo wa visiwani humo kwa gharama kubwa, nchi hizo zilianza kuneemeka kutokana na rasilimali itokanayo na visiwa hivyo.

Nchi hizo zilijenga miji mikubwa yakiwemo majiji ambayo yalitokana na rasilimali hizo za Visiwani ambapo Tawala zilizokuwepo zikavunjwa na kupandikiza watu wenye itikadi na mila za kwao ili watawale kwa manufaa ya wageni hao.

Wadanganyika na Wafitinika walilaghaiwa na hatimaye vyanzo vyote vya uchumi vikawa chini ya wageni ambao nao wakawa wanaitumia ile mali kwa kunufaisha nchi zao kwa kisingizio cha kuwekeza Vitegauchumi, Dhahabu, Almasi na baadhi ya vito vya thamani vilisafirishwa kwa wingi kupelekwa Ughaibuni.

Hatimaye vidani ambavyo vilikuwa vikitengenezwa visiswani humo vikawa vinaingizwa kutoka nchi za Ughaibuni kwa fedha za kigeni na hivyo kuifanya mali ya wananchiwa visiwa hivi kupotea taratibu ilhali raia wa visiwa hivi bado hawajatanabahi.

Waliendelea kujidanganywa na vijizawadi ambavyo vilikuwa havina maana yoyote visiwa hivi walidanganywa na vijizawadi vidogovidogo visivyokuwa na manufaa yoyote zawadi ambazo asili yake inatokana na visiwa vyao.

Utamaduni wa nchi za kigeni ulizidi kujikita ndani ya visiwani hivi klabu za pombe mbalimbali zilijengwa majumba na madanguro ambayo watu hutembea uchi kama wanyama nyakati za usiku vilizidi kushamiri.

Ufukwe wa bahari ambao hapo awali ulikuwa ni sehemu muhimu kwa watu kupumzika na kupunga hewa ulibadilika na kuwa ni sehemu za maasi na uasherati na kwamba lilikuwa ni jambo la kawaida kuwakuta watu wa jinsia tofauti wakiwa pembezoni mwa bahari mithili ya wanyama walifanya vitendo vya ngono hadharani huku wakiwa kama walivyotoka matumboni mwa mama zao.

WADANGANYIKA walidanganyika na kuacha uchamungu wao kwa kuzamia kwenye maadili ya kishetani, maadili ambayo yaliacha athari mbaya kwa vizazi hadi vizazi ambapo,Wafitinika walifitinishwa na ndugu zao Wadanganyika kiasi kwamba uhusiano wao ulikuwa mbali kama mbingu na ardhi ile hali ya awali ya kukutana baina ya visiwa hivi na kujadiliana mustakabali wa visiwa vyao ilitoweka.

Inaendelea…..

Fasihi(AZIMIO LA DODOMA)

15 04 2006

La Dodoma azimio, Makene limetulia,
Lafaa kuwa zingatio,Bloguni kutumia,
Tena liwe karipio, watakao vurugia,
Azimio la Dodoma,liwe la wanaBlogu.

Kwa uhuru twandikia, wengi wanatusomea,
Maadili kupindia, hako wa kutukemea,
Uhuru tunotumia, sote twaushere’kea,
Azimio la Dodoma,liwe la wanaBlogu.

Sheria kuiwekea, madhara kutukingia,
Uhuru uliopea,majina twajiandikia,
Msaliti kitokea,Blogu tutakimbia,
Azimio la Dodoma, liwe la wanaBlogu.

Wazo lenu wa Dodoma,mkono naliungia,
Kikao chenu ni dhima,ni mfano kuigia,
Fikira hazitokoma,wanaBlogu kuchangia,
Azimio la Dodoma, liwe la wanaBlogu.

Miruko,Kazonta,Mtangoo,jema mlofikiria,
Msaki, Msangi katika mtandao, wote wanalichangia,
Nyembo,Ndesanjo,na wengineo,hima wanaliwania,
Azimio la Dodoma, liwe la wanaBlogu.

Adabu kuzingatia, katika kuandikia,
Maadili kufatia, ya uandishi Blogia,
Wasomao jifunzia,kazi zilizotulia,
Azimio la Dodoma, liwe la wanaBlogu.

Wakatabahu kuungia,beti saba natulia,
Hima sote kubalia,la Dodoma liwe njia,
Kwamba si nadharia, kwa vitendo fuatilia,
Azimio la Dodoma,liwe la wanaBlogu.

Ndimi Mkwinda Rashid, kalamu naiachia,
Kamwe sina ukaidi,kwa hili kuliungia,
Nitafanya tashdidi, wengi kuwashawishia,
Azimio la Dodoma, Liwe la wanaBlogu.